Saturday, September 26, 2015

MUZDALIFA YAENDELEZA KUENEZA MSAADA PEMBA

Jumuiya ya Muzdalifa yasaidia wananchi wa Pemba na watoto mayatima


JUMUIYA ya Kiislam ya Muzdalifa Charitable  Association Ofisi ya Pemba imechimba ng’ombe mia moja na ishirini (120)  na kuwapa sadaka wananchi wa Kisiwa cha Pemba wakiwemo watoto yatima .
Uchinjwaji wa ng’ombe hao umeenda sambamba na kusherekea sikuu ya Idd El Hajj inayosherekewa na waumini wa dini hiyo baada ya kukamilika kwa Ibada ya Hijja huko Macca.
Akizungumza  na mwandishi wa habari Mratibu wa Jumuiya hiyo Pemba Omar Hassan  amesema kuwa Jumuiya  yake imepokea msaada wa ng’ombe hao kutoka Jumuiya marafiki zilizoko Nchini Uturuki .
Amefahamisha kwamba kila mwananchi atafaidika na msaada wa nyama mijini na vijiji ambapo Jumuiya huwafikishia wananchi popote walipo bila a kujali imani ya dini , vyama wala kabila .
“Hii ni sadaka na inatakiwa kuwafikia waislamu wote , sisi Jumuiya tumepokea kutoka Jumuiya mbili  marafiki zilizoko Nchini Uturuki  , tunatoa bila ubaguzi pia tumewalenga zaidi watoto yatima ”alifahamisha .
Omar amewataka wananchi kutambua kwamba sadaka hiyo imetolewa kwa ajili yao , hivyo wanatakiwa kushirikiana na Jumuiya katika kufanikisha ugawaji wa sadaka na wale ambao hawatabahatika kupata waelewe kwamba haikuwa ridhiki yao .
“Tunawaomba wananchi kushirikiana na Jumuiya , na tunatambua kutokana na jiografia ya Kisiwa cha Pemba baadhi ya maeneo hawatayafikia , hivyo wale ambao hawatabahatika waelewa haikuwa bahati yao ”alieleza .
Nao baadhi ya wananchi waliokutwa na mwandishi wa habari hizi katika eneo la machinjio ya Wete , wameishukuru Jumuiya hiyo kutokana na msaada huo na kusema  kuwa umekuja wakati muafaka .
Ali Khatib Chwaya akiwa katika chinjio hilo amesema kuwa Jumuiya hiyo imesaidia kukabiliana na changamoto ya kitoweyo kwa waumini wa Dini hiyo hasa katika kipindi hichi cha kusherekea Sikuu ya Idd El Hajj.
“Msaada huu umesaidia sana katika suala la kitoweyo hasa kwa watoto yatima na waislamu wengine wanaoishi kwenye mazingira magumu kwani umekuja wakati muafaka ”alisema Chwaya .
Aidha ameeleza kwamba wapo baadhi ya wananchi ambao wamekuwa wakirudi na kurudia kuchukua kitoweyo jambo ambalo linawafanya baadhi yao kukosa kupata sadaka hiyo ambayo imetolewa kwa wananchi wote .
Mchinjaji maarufu katika Mji Wete Shehe Haji amesema kuwa katika kusherekea Sikuu hiyo ya Idd El Hajj wamechimba ng’ombe sitini kwa siku ya kwanza na siku ya pili wakachinja ng’ombe sitini .
Kwa upande wake mkaguzi wa nyama kutoka Idara ya Mifugo Rashid Hamad ameeleza kwamba ng’ombe wote waliochinjwa walikuwa na afya njema na walikuwa wanafaa kwa matumizi ya binadamu .

Aidha mkaguzi huyo wa nyama  amewatoa hofu wananchi juu ya usalama wao kwa kusema kwamba ng’ombe wote waliochinjwa hawana madhara kwa watumiaji.
NA MOHAMED HEMED.

No comments: