STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 24.9.2015
SERIKALI ya
Mapinduzi ya Zanzibar na Serikaili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
zitaendelea kukabiliana na wale wote watakaofanya vitendo vitakavyoashiria
kutaka kuvunja amani ya nchi wakati wote hasa katika kipindi hiki cha Kampeni
za Uchaguzi Mkuu,wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo leo katika hotuba yake ya
Baraza la Idd al Hajj aliyoitoa huko katika ukumbi wa Chuo cha Amali Mkokotoni,
Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alhaj Dk. Shein aliwahakikishia wananchi
kuwa hakuna atakayeonewa au kudhulumiwa kwa njia yoyote ile lakini ni vizuri
wajue kuwa Serikali ina wajibu wa Kikatiba wa kuwalinda watu wote na mali zao
pamoja na wageni wanaoitembea Zanzibar.
Aidha, Alhaj Dk. Shein alitumia fursa
hiyo kuwakumbusha viongozi wa kisiasa, kijamii na wa madhehebu ya dini
kuwasisitiza wafuasi wao umuhimu wa kuilinda amani na kujiepusha na vitendo
vyote vitakavyoweza kuondoa amani na utulivu uliopo.
“Nimekuwa nikisema mara kadhaa kuwa amani
haina mbadala. Bila ya amani hatuwezi kupata maendeleo yoyote”,alisisitiza
Alhaj Dk. Shein.
Alhaj Dk. Shein alisema kuwa kutokuwepo kwa
amani kunahatarisha uhai wa watu na ni sababu ya kuharibu miundombinu ya aina
mbali mbali na kuzua fadhaa kwa jamii.
Aliendelea kueleza kuwa kutokuwepo kwa
amani huwaondolea wasaa hata waumini katika kutekeleza ibada za kumuabudu Mola
wao.
Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Shein alisema
kuwa Serikali imeanza kazi ya kufanya upembuzi yakinifu ili kuanzisha Mfuko wa
Hijja Zanzibar kwa lengo la kuwasaidia wananchi wengi zaidi waweze kupata fursa
ya kuitekeleza ibada ya Hijja kwa wepesi na mapema zaidi.
Alisema kuwa Mfuko utakapoanzishwa watu
wengi zaidi watapata nafasi na uwezo wa kuweka fedha kidogo kidogo kwa mujibu
wa uwezo wao na hatimae watamudu kutekeleza ibada za Hijja na Umra kwa mujibu
wa makubaliano na taratibu zitakazowekwa na Mfuko.
Aidha, Alhaj Dk. Shein alieleza kufarajika
kwake na hatua kubwa ya maendeleo iliyofikiwa katika Mkoa wa Kaskazini Unguja
katika sekta za kiuchumi, huduma za jamii na muamko wa wananchi katika
kuzitumia fursa mbali mbali za kujiendeleza kiuchumi kwa kushirikiana na
serikali.
Alhaj Dk. Shein alisema kuwa katika
kuhakikisha kuwa Mikoa inazidi kuimarika kiuchumi, kuongeza fursa za ajira hasa
kwa vijana na kuimarisha upatikanaji mzuri wa huduma za jamii, Serikali
imeazimia kujenga mji wa kisasa katika Mkoa huo kwenye vijiji vya Matemwe na
Kijini.
Pia, alisema kuwa ujenzi wa barabara
wenye urefu wa kilomita 20.2 kutoka Matemwe kupitia Kijini hadi Kidoti
umekwishaanza.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alisema kuwa
wananchi wengi wa maeneo ya Bumbwini, Mkokotoni, Bwekunduni, Fungurefu na
vijiji vyengine vya Mkoa huo wameimarisha uchumi wao kwa kujishughulisha na
biashara ya madagaa ambayo husafirisha hadi Kongo na nchin nyengine Jirani.
Akieleza mafanikio yaliofikiwa katika
kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika Mkoa huo Alhad
Dk. Shein alisema kuwa upatikanaji wa
huduma hiyo imefikia asilimia 71.68.
Alisema kuwa mafanikio hayo yamefikiwa
baada ya kutekeleza miradi mikuu mitatu ya maji safi na salama katika Mkoa huo
ukiwemo Mradi wa Serikali kupitai Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), Mradi wa
Ras-al-Khaiman na ADB.
Kadhalika Alhaj Dk. Shein alisema kuwa
Serikali imeimarisha huduma za hospitali ya Koteji ya Kivunge pamoja vituo vya
afya vyengine katika Mkoa huo ili kuziimarisha afya za wananchi.
Alhaj Dk. Shein alitumia fursa hiyo
kuzitaka taasisi zinazoshughulikia usafi wa miji ziongeze kasi katika kusafisha
misingi ya maji machafu na njia za maji na usafi wa mazingira ili kuepukana na mardhi katika kukabiliana na
mvua za vuli zijazo ambapo kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa upo uwezekano
wa kuwepo mvua kubwa za ‘El-Nino’.
Pia, Dk. Shein aliwanasihi wananchi
kuacha kujenga katika sehemu za mabonde na wote wawe na moyo wa kusaidiana
wakati wote, hsa pale Mwenyezei Mungu anapoleta mitihani mabali mbali.
Aidha, Alhaj Dk. Shein aliutaka uongozi
wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na
taasisi zinazowasimamia madereva wachukue hatua madhubuti katika kukabiliana na
tatizo la ajali za barabarani katika Mkoa huo.
Mapema Alhaj Dk. Shein aliungana na wananchi
katika Sala ya Idd-El-Hajj huko Katika uwanja vya Mpira Mkokotoni ambapo
viongozi mbali mbali walihudhuria katika ibada hiyo pamoja na Baraza la Idd
akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu Pili Balozi Seif
Idd na viongozi wa dini, siasa, Serikali pamoja na wananchi.
No comments:
Post a Comment