MGOMBEA
nafasi ya urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
ameahidi ndani ya miaka miwili kukamilisha mpango mkubwa wa kuimarisha sekta ya
uvuvi utakaojumuisha kuwapatia wavuvi boti maalum za kufanyia shughuli za uvuvi.
Amesema mpango huo
ambao matayarisho yake tayari yameanza utashirikisha sekta binafsi ambapo
tayari makubaliano ya awali yamefanyika ambapo katika hatua ya awali boti 20
kumi zikiwa za mita 6 na nyingine 10 za mita 9 watapewa wavuvi kwa majaribio.
Akizugumza katika
mkutano wa kampeni uliofanyika katika kiwanja cha Shamemata huko Micheweni,
Mkoa wa Kaskazini Pemba, Dk. Shein alieleza kuwa endapo wavuvi watazikubali
boti hizo baada ya majaribio boti nyingine zaidi zitatengenezwa na kupewa
wavuvi.
Dk. Shein alifafanua
kuwa baada hatua hiyo kukamilika itafuata hatua nyingine ya ujenzi wa boti za
ukubwa wa zaidi ya mita 18 kwa ajili ya uvuvi wa bahari kuu hivyo kutoa fursa
kwa wavuvi wa Zanzibar kuvuna rasilimali hiyo muhimu kwa uchumi wa nchi.
“Tunaamini kuwa
tunaweza kuwawezesha kuvua samaki eneo la bahari kuu ndani ya miaka mitano kwa
kushirikiana na kampuni moja kubwa ya kutengeneza boti na meli za uvuvi ya Sri
Lanka” Dk. Shein aliwaambia wananchi hao waliokuwa wakimshangilia.
Katika mkutano huo
Dk. Shein ambaye anagombea nafasi hiyo kwa mara ya pili baada ya kumalizika
kipindi chake cha kwanza cha miaka mitano amewataka wananchi kumchagua tena ili
kupata fursa ya kuendeleza mipango ya kujenga Zanzibar.
No comments:
Post a Comment